JINSI YA KUANZA BIASHARA NA MTAJI MDOGO

Watu wengi wamekuwa wakitamani kuanza biashara lakini wanafikiri namna ya kuanza kwani mtaji wao ni mdogo sana.
Usiogope; kuwa na mtaji mdogo au kutokuwa nao kabisa sio mwisho wako wa kutimiza malengo yako.
“Usilie juu ya kile ambacho huna; tumia vizuri kile ulichonacho.”

Reginald Mengi
Zipo mbinu mbalimbali ambazo zinaweza kukuwezesha kufanya biashara hata kama utakuwa na mtaji mdogo. Tafadhali fuatilia hoja jadiliwa hapo chini kwa ufafanuzi zaidi.

1. Kuwa mbunifu

Moja kati ya mambo ambayo yatakusaidia sana kwenye kuanza biashara kwa mtaji mdogo ni ubunifu. Kwa njia ya ubunifu utaweza kushinda biashara na bidhaa zilizoko sokoni kwa urahisi zaidi. Unaweza kufanya haya yafuatayo:
  • Chagua wazo la biashara unalolipenda na kuliweza vyema. Hili litakusaidia kukabili changamoto vyema.
  • Angalia tatizo au uhitaji uliopo sasa na uutatue kwa bidhaa au huduma yako.
  • Panga bei vizuri; unaweza kuweka bei ambayo ni tofauti kidogo na bidhaa au huduma ambazo tayari ziko sokoni ili uwavutie wateja.
Kwa kufanya mambo yaliyoelezwa hapa juu utaweza kukuza biashara na mtaji wako kwa muda mfupi zaidi.

2. Anza na unachokijua

Unapokuwa na mtaji mdogo huhitaji kuhusisha mambo mengi mageni au yanayotegemea sana watu wengine kwa kuwa huna pesa za kuyagaramia.
Kwa mfano kama unaanzisha biashara ya ushonaji basi anza kutengeneza mavazi yale unayoyaweza kwa kutumia vifaa ulivyonavyo; kwa njia hii utajenga mtaji wako kisha baadaye utaweza kuajiri wengine watakao kuwezesha kutengeneza aina nyingine zaidi.
Unapofanya kile unachokijua gharama huwa haziwi kubwa sana kwani ni kitu unachokimudu mwenyewe.

3. Waambie watu unachokifanya

Waambie watu unachokifanya kwani hili litakuwezesha kupata wateja na kufahamika. Watu wakijua unachokifanya watatamani kukifahamu zaidi; hili litakuwezesha kupata wateja na kuongeza mtaji wako.
Usiogope kueleza kuwa unafanya biashara ya mboga, chakula, duka dogo la bidhaa n.k. Kwani hujui unaemweleza atakuwa nani kwenye biashara yako.
Ukiwa na marafiki kwenye mitandao ya kijamii waeleze pia juu ya kile unachokifanya.

4. Epuka gharama zisizokuwa za lazima

Kwakuwa bado una mtaji mdogo jitahidi kuepuka garama zisizo za lazima kama vile ofisi ya kifahari, matangazo ya gharama kubwa n.k.
Kuwa na matumizi mazuri ya fedha hasa kwa mambo ya msingi tu. Watu wengi wameshindwa kwenye biashara kwa sababu wameanza biashara kwa mbwembwe za matumizi badala ya huduma bora zenye ubunifu.

5. Fanya kazi kwa bidii

Kamwe huwezi kuona mafanikio kama hutofanya bidii. Kumbuka wewe ni mjasiriamali anayeanza hivyo ni lazima ufanye bidii ili soko litambue kuwa upo pia unaweza. pia hakikisha unatoa huduma yenye ubora wa hali ya juu kwa bei ambayo wateja wataweza kuimudu. Jitese kwa muda mfupi kwa kipindi cha kuweka msingi wa biashara yako kwani hata kipindi cha kupanda katika kilimo huwa ni cha taabu.

6. Tumia rasilimali na fursa zilizopo

Njia nyingine itakayokuwezesha kuanza biashara ukiwa na mtaji mdogo ni kutumia fursa zilizopo. Kumbuka kuwa huwezi kutengeneza fursa kama huwezi kutumia fursa zilizopo.
Tumia fursa kama vile mitandao ya kijamii ili kujitangaza. Pia unaweza kutumia udhaifu uliopo katika biashara nyingine za watangulizi wako kama fursa kwani unaweza ukarekebisha udhaifu huo kupitia biashara yako.
Zipo pia fursa za mikopo yenye masharti nafuu ambayo itakuwezesha kuongeza mtaji wako. Kumbuka unahitaji kutumia mkopo kwa makini kwani utahitajika kuurudisha pamoja na riba tena kwa wakati.

7. Jali wateja

Kujali wateja katika biashara  ni jambo muhimu sana kama unataka kuona matokeo chanya. Siku zote ninapenda kusema “wateja hufugwa”. Wateja hufugwaje? Hufugwa kwa huduma nzuri.
Waheshimu wateja wako pia hakikisha unatimiza na kumaliza haja zao katika ubora wa hali ya juu. Kumbuka siku zote mteja huja kwanza kabla ya pesa; hivyo usitangulize pesa kabla ya huduma nzuri kwa mteja.
Ukilifanyia kazi hili utaweza kukuza biashara na mtaji wako kwa muda mfupi.

Hitimisho
Zilizojadiliwa hapa ni mbinu saba zitakazokuwezesha kuanza biashara na mtaji mdogo. Usiogope unaweza hata kama una kiasi kidogo sana cha fedha.
Thubutu, nza, fanya bidii, weka nidhamu, mtangulize Mungu na hakika utaona mafanikio chanya katika biashara yako.
“Anzia ulipo.Tumia ulicho nacho. Fanya unachoweza.”

Share on Google Plus

About Anonymous

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment